Ms Sarah Hermitage
KWA
takriban miaka mitano sasa, raia mmoja wa Uingereza, Sarah Hermitage
amekuwa akiendesha kampeni ya kumchafua Rais Jakaya Kikwete, Serikali ya
Tanzania, taasisi muhimu za nchi yetu kama vile mahakama, waandishi wa
habari na hata Watanzania ambao wamekua wakimpinga.
Pamoja
na kuwa kumekua na mapungufu katika serikali yake na vyombo vyake kama
ilivyo kwa serikali nyingine Duniani ikiwamo ya Uingereza, Muingereza
huyu amekua akitoa kashfa kwa kila jambo linaloandikwa ama kujadiliwa
kuhusiana na viongozi wa Tanzania na taasisi zake na kwa kutumia lugha
isiyo na staha.
Watanzania siku zote wakiwamo wanasiasa,
waandishi wa habari na wanaharakati, wamekua wakiikosoa na hata
kuishambulia serikali na vyombo vyake inapokosea jambo ambalo ni jema na
linasaidia kuimarisha utawala bora, lakini kwa staili anayotumia
Muingereza huyu ni kupitiliza mipaka na zaidi ya yote ni udhalilishaji
usioweza kuvumilika kwa mtu mwenye mapenzi mema na nchi yake.
Dhumuni
la Sarah Hermitage na washirika wake wakiwemo baadhi ya Watanzania ni
kuzishawishi nchi za Magharibi wakianzia na Uingereza kusitisha misaada
na uwekezaji katika Tanzania. Hilo angeweza kulifanya huko kwao kwa
kuwasiliana na serikali yake, lakini badala yake amekuwa akitumia
mitandao ya kijamii na barua pepe tena kwa kutumia lugha ya kukashifu na
kudhalilisha.
Watanzania wote tuna jukumu la kutetea heshima ya
nchi yetu, lakini wapo wale ambao tumewapa jukumu la kusimama mstari wa
mbele. Jambo la kusikitisha ni kwamba ni watu wachache sana kama Mbunge
wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe ambaye ambaye amekua na ujasiri wa
kumkabili Muingereza huyu, kwa kumwambia wazi kwamba kama ni misaada ana
haki ya kuishawishi nchi yake kuzuia misaada kwa Tanzania lakini si kwa
kudhalilisha Watanzania.
Zitto alienda mbali zaidi kwa kusema
kwamba nchi nyingi tajiri duniani ikiwamo Uingereza, zimejengwa kwa
kutumia rasilimali walizozipora katika nchi walizozitawala ikiwamo
Tanzania na kwamba nchi hizo zinaweza pia kuendesha shughuli zake bila
misaada ya dharau. Bahati mbaya sana watendaji wengine wengi ambao
wanapaswa kutetea heshima yetu, hili suala limewapita, pengine kutokana
na kutokua na taarifa sahihi ama kwa kutowajibika.
Jambo la
kujiuliza, wale ambao miongoni mwa majukumu yao ya kila siku ni kutetea
na kulinda hadhi na heshima ya nchi yetu wanafanya kazi gani? Sasa
tunawalipa mishahara mikubwa na marupurupu ya nini kama hawawezi
kututetea tunapodhalilishwa ama kutukanwa?
Hali hii inatufanya
tukumbuke ujasiri wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye mara
kadhaa aliwatunishia misuli viongozi wa mataifa makubwa walipotaka
kuidhalilisha nchi yetu, sembuse raia mmoja ambaye amekua akitumia
matatizo yake binafsi kutaka kuidhalilisha Tanzania na kutaka
kuishinikiza serikali yake na nyingine kuichukia Tanzania.
Jinsi anavyotumia mtandao wa twitter kuchafua Tanzania
Sarah
Hermitage amekua akitafuta katika taarifa za vyombo vya habari vya
ndani na nje ya Tanzania vinavyoandika taarifa zozote kuhusu Tanzania na
kuziongezea maneno ya kukashifu na kejeli.
Kwa mfano amekua
amechukua taarifa inayomunukuu Raia Jakaya Kikwete akiitaka Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kupambana na rushwa hadi ndani
ya Baraza la Mawaaziri, na yeye kuongezea maneno akisema, “kundi moja la
majambazi linaliambia kundi lingine la majambazi kukamata mwizi”.
Akachukua
taarifa iliyochapishwa katika vyombo vya habari ikimnukuu Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda akikaribisha wawekezaji katika kilimo na yeye kuongeza
maneno akisema, “Mheshimiwa Pinda kitakachoendelea kukandamizi uwekezaji
katika kilimo cha Tanzania ni uporaji wa ardhi ya wawekezaji katika
mtindo wa Mugabe (Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe).”
Amekua
akidiriki kukashifu hadi majaji wote wa Tanzania kwamba wana bei
akisema, “sina hakika kama unaweza kupata jaji ambaye si mla rushwa.
Wote wana bei,” kauli ambayo hata Watanzania wanakua wakiitoa kwa
uangalifu maana hata kama kuna majaji ambao si waadilifu, haiwezekani
wakawa ni wote, kama ilivyo katika taasisi nyingine.
Raia mmoja wa Kenya anayeishi Tanzania, aliyejitambulisha kwa jina la Marigi Patrick aliandika katika mtandao kwa kusema;
“Sisi
Wakenya tuna matatizo yetu na tumekua na tofauti kubwa sana za wazi
wazi, lakini anapotokea raia wa kigeni kumshambulia kiongozi wetu tena
kama Rais wa nchi, tunaungana na kumshughulikia. Kuna wakati Wazungu
walimshambulia Rais Mwai Kibaki, sote tukisaidiwa na wabunge wetu na
vyombo vya habari tulimshambulia hadi akakoma kutudharau.”
Marigi
ambaye anajihusisha na biashara ya bima, anasema Watanzania bado ni
wachanga katika demokrasia, ama wanadharau kila kitu bila kujua madhara
yake katika hadhi na heshima ya Taifa, na ndio maana wanashindwa
kutofautisha kati ya demokrasia na udhalilishaji unaofanywa na raia wa
nchi nyingine kama alivyo Sarah Hermitage.
Source: THE SILVER DALE CASE BLOG
Source: THE SILVER DALE CASE BLOG
No comments:
Post a Comment