Friday, January 20, 2012

 

INDONESIA KUPAMBANA NA WAKWEPA NAULI KWENYE TRENI


MAMLAKA za reli nchini Indonesia zimeamua kupambana na watu wanaokwepa kulipa nauli kwenye treni kwa kuning’iniza matufe ya zege katika madaraja juu ya reli hususani kwa wakwepaji ambao hupanda juu ya mapaa ya treni.
Kwa mujibu wa maofisa wa shirika la reli ambalo ni la umma, matufe hayo yenye umbo la mipira lakini yaliyotengenezwa kwa zege yatakomesha watu wanaohatarisha maisha yao kwa kusafiri wakiwa nje kwenye mapaa ya treni.
Msemaji wa shirika hilo, P.T. Kerea Api alisema: “Tumefanya kila kitu mpaka kuweka seng’enge za miiba lakini haikuwezekana, labda hatua hii itafanikiwa.”
Hatua za kupambana na watu hao zimekuwa zikigonga mwamba kila mara ambapo wakwepa nauli hao wamekuwa wakiwashambulia maofisa wa reli kwa mawe, na pale ambapo walijaribu kuweka matufe mara ya kwanza, nyaya za kuyaning’iniza zilikuwa fupi mno kiasi hayakuweza kuwafikia wadandiaji.
Hivyo, watu watabidi kuchagua kulipa nauli au kubondwa na matufe hayo.


Muhammad Ali atimiza miaka sabini


Ustadh, haiba na misimamo isiyoyumba ya Muhammad Ali ndio mambo yaliyosaidia kuufanya mchezo wa masumbwi kuwa maarufu duniani siku ya leo anatimiza miaka sabini (70)


Papiss Demba ajiunga na Newcastle


Mshambuliaji raia wa Senegal Papiss Demba Cisse amejiunga na klabu ya Newcastle United akitokea Freinburg inayocheza ligi ya Ujerumani- Bundesliga kwa mkataba wa miaka mitano na nusu, kwa kitita ambacho hakijaelezwa.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26 amekubali uhamisho huo kabla hajajiunga na timu yake ya taifa kwa ajili ya Kombe la Mataifa ya Afrika, ambapo atakuwa sambamba kuongoza mashambulizi na Demba Ba katika kikosi cha
Senegal.
Meneja wa Newcastle Alan Pardew amekiri: "Tangu alipoondoka Andy Carroll, Papiss alikuwa chaguo langu la kwanza katika nafasi hiyo muhimu ya ushambuliaji."
Mkurugenzi mtendaji wa Newcastle Derek Llambias ameongeza: "Tunafuraha kubwa tumempata Papiss.


Hasira kwa 'mashambulio ya suruali' Malawi

                       Rais wa Malawi Dr Bingu wa Mutharika

Takriban watu 3,000 wamekusanyika Blantyre nchini Malawi kupinga mashambulio dhidi ya wanawake wanaovaa suruali.
Baadhi ya wachuuzi wa kike wiki hii walipigwa na kuvuliwa nguo kwenye mitaa ya mji mkuu, Lilongwe, na Blantyre kwa kutovaa mavazi ya asili.
Mmoja aliyeandaa maandamano hayo ameiambia BBC amewasihi wanawake kujitokeza wakiwa wamevaa suruali na fulana nyeupe kuonyesha kukasirishwa kwao.
Rais Bingu wa Mutharika alisema kupitia redio ya taifa kuwa wanawake wana haki ya kuvaa wanachotaka.
Alikana taarifa kuwa aliamuru wanawake waache kuvaa suruali.
Mpaka mwaka 1994, wanawake kwenye nchi hiyo ya kusini mwa Afrika yenye misimamo mikali walikatazwa kuvaa suruali au sketi fupi chini ya uongozi wa kidikiteta wa Hastings Banda.
Wanaume pia walikatazwa kuwa na nywele ndefu.
Wanawake pia wameshambuliwa kwa kuvaa suruali katika nchi za Kenya, Afrika Kusini na Zimbabwe katika miaka ya hivi karibuni.

'Kukatishwa tamaa kutokana na hali ya uchumi'

Mwandishi wa BBC aliyopo Blantyre Raphael Tenthani alisema makamu wa Rais Joyce Banda, waziri wa jinsia, wabunge kadhaa, wahadhiri wa chuo kikuu na wanaharakati walihudhuria maandamano ya Ijumaa.
Seodi White, mwanasheria na mwanaharakati wa haki za wanawake na aliyeandaa maandamano hayo, alisema wanawake hao hawakuvaa mavazi yasiyo ya heshima.
Ndio Malawi ni nchi yenye msimamo mkali. Lakini tumekuwa tukivaa tunavyotaka, kwa kiwango cha heshima inayotakiwa, ambayo ni kiwango cha watu wote duniani, kwa miaka 18. Na hakuna anayeweza kusimama akasema ni kinyume na Wamalawi, " alikiambia kipindi cha Network Afrika cha BBC.
Alisema wanawake walikuwa wakilengwa na vijana ambao hawafurahishwi na hali ya kiuchumi nchini humo.
"Wachuuzi unaowaona mitaani si watu wazima. Hawa ni vijana, wadogo wa kuwa hata umri wa watoto wangu.
"Wananieleza mimi kuhusu utamaduni? Wananiambia mimi namna ya kuvaa?
"Hivi hili suala kweli ni kuhusu utamaduni au kitu kingine kinachohusiana na hali ngumu ya uchumi wanayokubaliana nayo watu wakitafuta namna ya kutoa hasira zao?
Awali, Bi Banda pia alilaumu mashambulio hayo kutokea kutokana na uchumi nchini Malawi, ambapo kwa sasa kuna upungufu mkubwa wa mafuta na fedha za kigeni.

1 comment: