Saturday, August 11, 2012

TASWIRA ZA PAPAA MUSOFE ALIPOFIKISHWA MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI KISUTU LEO KWA TUHUMA ZA MAUAJI

Marijani Abubakar Msofe ‘Papaa Musofe’ (58) akiingia kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo, kwa ajili ya kusomewa mashitaka katika kesi ya mauaji inayomkabili
 Papaa Musofe akiandikisha jina kwa maofisa wa Polisi mahakamani hapo
 Papaa Musofe akipandisha ngazi za mahakama ya Kisutu kwenda kusomewa shitaka la tuhuma za mauaji
 Papaa Musofe akipanda gari ya polisi kurejea mahabusu baada ya kusomewa shitaka la mauaji kwenye mahakama ya Kisutu
Papaa Musofe wa pili kulia, akiwa amekaa kwenye gari ya polisi chini ya uangalizi mkali, tayari kwa safari ya kurudi mahabusu.Picha Kwa Hisani Ya Habari Mseto Blog

AJALI YA GARI ILIYOUA RAIA 11 WA KENYA ENEO LA WAMI LEO

Baadhi ya wakazi wa kitongoji  cha Makole Mkoa wa Pwani wakiangalia ajali ya gari iliyotokea leo katika eneo la Mto Wami na kusababisha vifo vya watu 11 wote wakiwa raia wa Kenya. 
 Basi lililokuwa limewabeba raia wa Kenya waliokuwa wakielekea jijini Dar es salaam kwa ajili ya mikutano ya injili  likiwa limetumbukia katika korongo jirani na Mto Wami na kuua watu 11 katika Kijiji cha Makole Mkoa wa Pwani.
Baadhi ya abiria walionusurika wakiwa katika eneo la tukio kabla ya kupata msaada.Picha Kwa Hisani Ya Habari Mseto Blog

African Lyon yatambulisha kocha mpya kutoka Argentina

Kocha mpya wa timu ya African Lyon inayoshiriki  Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Pablo Ignacio Velez  kutoka Argentina wa kwanza kulia, akizungumzia nini atafanya akiwa  na timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao uliopangwa kuanza Septemba Mosi mwaka huu. Kocha huyo amesaini mkataba wa miaka mitatu na timu hiyo. Wengine katika picha ni Charles Otieno ambaye ni mkurugenzi wa ufundi na Biashara wa timu hiyo.
****
Mwandishi wetu
KOCHA mpya wa timu ya soka ya African Lyon, Pablo Ignacio Velez, amewasili nchini tayari kuanza kuinoa timu hiyo na kuomba apewe muda wa kukisuka upya kikosi hicho huku akiahidi mabadiliko zaidi ya soka kwenye timu hiyo.

Pablo raia wa Argentina aliyasema hayo jana baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia timu hiyo na kusisitiza lengo lake kubwa ni kuhakikisha vijana wanapewa nafasi ya kuonyesha vipaji vyao na ndivyo itakavyokuwa Afrika Lyon.

"Sikuja Tanzania kutafuta pesa, ndoto yangu kubwa ilikuwa kufundisha soka barani Afrika hivyo wakati ni sasa," alisisitiza kocha anayezungumza lugha ya 'kiispanyola'.

Pablo alisema "kazi ya aina yoyote lazima ipewe muda na mchezaji lazima atengenezwe hivyo watanzania wawe na subira kwa ajili ya kupata matunda mazuri ya vijana hapo baadae kutoka African Lyon.

Kocha huyo aliyewai kuzichezea timu za taifa za vijana chini ya miaka 17 na 20 za Argentina hakusita kusisitiza suala la nidhamu kwa wachezaji wa timu hiyo ya ndani na nje ya uwanja.

"Nidhamu ni muhimu kwa wachezaji wangu cha msingi tushirikiane katika kufanikisha hili kwa vijana kwani mchezaji anatakiwa kati ya miaka 18 na 19 awe ametengeneza jina kupitia soka ,"  alisema Pablo.

Naye Mmiliki wa African Lyon, Rahmu Kangezi alisema lengo la kumleta kocha huyo ni kuhakikisha timu hiyo inajongea mbele zaidi.

Kangezi alisema licha ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja lakini wanaweza kumtumia Pablo kwa kipindi kirefu kulingana na mfumo wa kuhakikisha wanaendeleza vijana katika timu yao.

"Pablo ni zaidi ya kocha, ana uwezo pia amecheza mpira pia ni kocha wa kwanza kutoka Argentina kuja Tanzania hivyo tunaimani timu yetu ya African Lyon itafika mbali zaidi kisoka," alisitiza Kangezi.

Pablo mwenye miaka 38 aliyechukua mikoba iliyoachwa na Jumanne Chale amewai kuifundisha  klabu ya Atletico Colo Colo De Chile (1998).

Klabu nyingine alizowai kufundisha ni Atletico Calchin (2000), Atletico Belgrano De Cordoba (1997), Atletico River Plate (1993-1995).

Klabu nyingine ni Banco De Cordoba (1991 na 1997), Deportivo Lasallano (1992) Atletico Argentino Penarol kwa miaka minne na klabu nyingine nyingi za Hispania na Argentina.

RAIS KIKWETE KATIKA MAZISHI YA RAIS JOHN ATTA MILLS WA GHANA

Shughuli mbalimbali za  mazishi za aliyekuwa Rais wa Ghana Profesa John Evans Atta Mills katika uwanja wa Independence Square jijini Accra leo Agosti 10, 2o12
 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na viongozi wenzie  baada ya shughuli ya mazishi ya Rais John Evans Atta Mills wa Ghana jijini Accra leo Agosti 10, 2012
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisaini kitabu cha maombolezo wakati shughuli ya mazishi ya Rais John Evans Atta Mills wa Ghana katika ukumbi wa Mikutano wa Ghana jijini Accra leo Agosti 10, 2012
 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akitoa heshima kwa aliyekuwa Rais wa Ghana Marehemu Profesa John Evans Atta Mills katika ukumbi wa Mikutano wa Ghana jijini Accra leo Agosti 10, 2012.PICHA NA IKULU

Tume ya Huduma za Bunge la Malawi yakutana na Spika wa Bunge la Tanzania mjini Dodoma

Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Anne Makinda (kushoto) na Naibu Spika Mhe. Job Ndugai (Mb) kwa pamoja wakiwa na mazungumzo ya kina leo na ujumbe wa Tume ya Huduma za Bunge la Malawi ulioko nchini hivi sasa, ambapo pamoja na mambo mengine walizungumzia uhusiano mzuri wa mabunge ya nchi mbili hizi. Kushoto kwa Mhe. Ndugai ni Naibu Spika wa Bunge la Malawi Mhe.Juliana Mpande (Mb) ambaye ni mkuu wa msafara. Wengine ni Kamishna  Alfred Mwechumu (Mb) na Kamishna Christina Chiwowo (Mb).
Spika wa Bunge la Tanzania akiwa na mazungumzo na Uongozi wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliofika ofisini kwake Dodoma leo. Spika Makinda amewataka na kuwaasa kuwa na uzalendo kwa nchi yao.Picha na Prosper Minja - Bunge

TAFF YATOA TAMKO JUU YA MAHARAMIA WA FILAMU

 Mwenyekiti wa Bongo move Jacob Stevin 'JB' kushoto akizungumza na waandishi wa habari Dar es salaam leo juu ya wizi mkubwa uliotokea hivi karibuni uliofanywa na Kampuni ya Steps Entatainmenti kwa kushirikiana na wasanii wwenyewe na kudai kuwa tabia hii ikomeshwa kwa maalamia wa kazi za wasanii kulia ni Msanii Vicent Kigos 'Ray' na Mwenyekiti wa Shilikisho la Filamu Tanzania 'TAFF' SIMON Mwakifwamba
Msanii wa Filamu Nchini Mohamed Nice 'Mtunisi' kushoto akizungumza na waandishi wa habari wakati walipokuwa wanatoa tamko lao kwa waandishi wa habari kuwa wameungana kupambana na maalamia wa kazi zao za sanaa kushoto ni  Mkurugenzi wa Msama Promotion, Alex Msama na msanii Muhsin Hawadh.Picha na www.burudan.blogspot.com
 ..........................
SHIRIKISHO la Filamu nchini(TAFF) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) pamoja Kampuni za usambazaji wa filamu na kazi za wasanii ‘wameapa’ kupambana na maharamia wote wa kazi hizo ili kulinda maslahi ya wasanii.

Wakizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam jana, umoja huo kwa pamoja ulisema umefika wakati tatizo la wizi wa kazi za wasanii lishughulikiwe kikamilifu ili kuzima mianya yote ambayo ni kero kwa muda mrefu.
Rais wa Shirikisho hilo Simon Mwakifwamba, mbali na mikakati hiyo pia aliiomba Serikali kutekeleza ahadi yake ya kuwasaidia wasanii kwa kupambana na maharamia hao aliodai kuwa wapo kila pembe ya nchi hii huku wakijiamini kwa kuendelea na kazi hiyo.

“Umefika wakati kwa Serikali kusikia kilio hiki cha wasanii na kuweka mbinu kali zitakazosaidia kuokoa maisha ya wasanii wanaoendelea kuwa masikini kila kukicha kutokana na uwepo wa watu wachache wanaoiba kazi zao”  “Tuna imani kuwa kama kazi za wasanii zitasimamiwa vizuri, tutaweza kuongeza pato la Taifa kwa kiwango kikubwa ikizingatiwa kuwa sanaa hii kwa sasa hapa nchini imeonyesha mafanikio isipokuwa kuna watu wachache ndiyo wananufaika nayo” alisema Mwakifwamba.

Naye Mwenyekiti wa Bongomuvi Jacobo Steven ‘JB’ alisema sanaa inaweza kuwa na nafasi ya tatu kwa kuchangia pato la Taifa ukiacha pato linalochangiwa na sekta za madini maliasili pamoja na utalii.

Alisema Serikali inapswa kuonyesha makali yake kwa kuwakamata wahusika wote wa wizi wa kazi hizo ili kuendeleza nguvu za wasanii wa hapa nchini walioamua kujitoa mughanga kufanya kazi zao.

Kwa upande wake Meneja usimamizi kutoka TRA Msafiri Ndimbo alisema Mamlaka hiyo imejipanga kudhibiti wizi wa kazi hizo kuanzia Januari Mwakani hasa baada ya Serikali kupitia Bunge lake kukubaliana kuweka mikakati ya kupamba na suala hilo. 
Ambapo wasanii na wasambazaji wa kazi zao wameungana pamoja kwa ajili ya kuhakikisha kazi zao zinakwenda kwa haki ili wasanii na kazi zao

UDOM YAPIGWA TAFU NA KAMPUNI YA TIGO KWA MSAADA WA VITABU 300

 Makamu Mkuu Wa Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) Elimu, Utafiti na Ushauri (Katikati) Prof Ludovick Kinabo akiwashukuru wawakilishi wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Tigo Kwa MSaada wa Vitabu hivyo. Pembeni kulia ni Meneja uhusiano na Udhamini wa Tigo Bw Edward Shila na Kushoto ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Tigo Kanda ya Kati Bi Fadhila Saidi
 Meneja Uhusiano na Udhamini wa Tigo Bw Edward Shila (Katikati) akionyesha maboksi yenye vitabu 300 ambavyo vimetolewa na kampuni ya simu za mikononi za tigo kwa Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM).
Naibu Makamu Mkuu wa Elimu, Utafiti na Ushauri wa Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) Prof Ludovick Kinabo (katikakati) Akipokea msaada wa Vitabu Kutoka Kwa Meneja Uhusiano na Udhamini wa Tigo Bw Edward Shila wakati wa makabidhiano ya Vitabu Hivyo vilivyotolewa na Tigo Chuoni hapo.

Ngorongoro Heroes wawasili salama Kwara-Nigeria

Ngorongoro Heroes, timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 imewasili asubuhi hii (Agosti 10 mwaka huu) kwa ndege ya Overland Airways kwenye mji wa Ilorin, Jimbo la Kwara lililo Kusini mwa Nigeria tayari kwa mechi ya marudiano dhidi ya wenyeji Flying Eagles itakayochezwa Jumapili.

Mechi hiyo ya raundi ya pili ya michuano ya U20 ya Afrika itachezwa kwenye Uwanja wa Township kuanzia saa 10 kamili jioni kwa saa hapa ambapo Tanzania itakuwa ni saa 12 kamili jioni. Ngorongoro Heroes ilitua jana (Agosti 9 mwaka huu) jijini Lagos ambapo ililala kabla ya kuja hapa.

Msafara wa Ngorongoro Heroes wenye watu 27 ukiongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mtwara (MTWAREFA) ulipokea na Ofisa Ubalozi wa Tanzania nchini Nigeria, Jones Mndeme na viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nigeria (NFF) umefikia hoteli ya Kingstone Grand Suites.

Kwa mujibu wa Kocha wa Ngorongoro Heroes, Jakob Michelsen, timu itafanya mazoezi leo jioni (Agosti 10 mwaka huu) wakati mazoezi ya mwisho yatakuwa kesho jioni (Agosti 11 mwaka huu) kwenye uwanja ambao utatumika kwa mechi ya Jumapili.

Wachezaji wote wako katika hali nzuri isipokuwa Issa Rashid na Aishi Manula ambao walikuwa wakisumbuliwa na tumbo baada ya timu kufika jana (Agosti 9 mwaka huu) jijini Nairobi, Kenya ambapo ilibadili ndege kuja Nigeria. Hata hivyo, hali zao zinaendelea vizuri na huenda wakawa sehemu ya kikosi cha kwanza kitakachoivaa Flying Eagles.

Mbali ya Rashid na Manula, wachezaji wengine walioko hapa kwenye kikosi cha Ngorongoro Heroes ni Barwany Khomeiny, Samir Ruhava, Dizana Yarouk, Leonard Muyinga, Hassan Ramadhan, Jamal Mroki, Omari Kheri, Frank Domayo, nahodha Omega Seme, Abdallah Kilala, Hassan Dilunga, Ramadhan Singano, Simon Msuva, Said Zege, Atupele Gren na Ramadhan Salum.

Mbali ya Michelsen, Benchi la Ufundi linaundwa na Mohamed Rishad 'Adolf' (Kocha Msaidizi), Peter Manyika (Kocha wa makipa), Nassoro Matuzya (Daktari), Joakim Mshanga (Physio), Juma Kizwezwe (Mtunza vifaa) na Meneja wa timu John Lyimo.

Flying Eagles ambayo ilishinda mechi ya kwanza mabao 2-1 nayo tayari imeshaingia hapa Ilorin ikitokea Lagos kwa mechi hiyo ambayo matokeo yake yataamua timu ipi itaingia raundi ya tatu ambayo ni ya mwisho kabla ya fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 zitakazofanyika mwakani nchini Algeria. Timu itakayovuka itacheza raundi hiyo na mshindi kati ya Congo Brazzavile na Afrika Kusini.

TUKIO LA KUUNGUA KWA DALADALA BUGURUNI DAR

 Gari ya Abiria aina ya Isuzu Journey, linalofanya kazi za kusafirisha abiria (Daladala)  likiteketea kwa moto jana mchana maeneo ya Buguruni Rozana jijini Dar es salaam. Chanzo cha moto huo hakikuweza kufahamika mara moja na katika ajali hiyo ya moto hakuna aliyejeruhiwa wala kupoteza maisha. Picha na Mpiga Picha wetu

WENGI WAZIDI KUNUFAIKA NA PROMOSHENI YA "JENGA MAISHA YAKO NA NMB"

Meneja wa Benki ya NMB, Kanda ya Dar es Salaam, Salie Mlay (kushoto) akibofya kwenye kompyuta kuwapata washindi wa promosheni ya 'Jenga Maisha Yako na NMB' katika droo iliyofanyika, Dar es Salaam jana, ambapo baadhi ya washindi watazawadia mabati, saruji, ada ya shule, mteja kuongezewa amana maradufu na zawadi nyingine lukuki. Wanaoshuhudia ni Mratibu wa Miradi wa Selcom Wireless, Everline Simpilu (kulia) na Sadiki Elimsu ambaye ni Mkaguzi Mwandamizi wa Bodi ya Kusimamia Michezo ya Kubahatisha (GBT)
Meneja wa Benki ya NMB, Kanda ya Dar es Salaam, Salie Mlay (kushoto) akibofya kwenye kompyuta kuwapata washindi wa promosheni ya 'Jenga Maisha Yako na NMB' katika droo iliyofanyika, Dar es Salaam leo.
Meneja wa Benki ya NMB, Kanda ya Dar es Salaam, Salie Mlay (kushoto) akibofya kwenye kompyuta kuwapata washindi wa promosheni ya 'Jenga Maisha Yako na NMB' katika droo iliyofanyika, Dar es Salaam jana, ambapo baadhi ya washindi watazawadia mabati, saruji ada ya shule, mteja kuongezewa amana maradufu na zawadi nyingine lukuki. Wanaoshuhudia ni Mratibu wa Miradi wa Selcom Wireless, Everline Simpilu PICHA ZOTE NA KAMANDA MWAIKENDA

No comments:

Post a Comment