Tuesday, January 31, 2012




UJUMBE WETU WA LEO








Dk. Shein akutana na Mwakilishi Mkaazi wa UN nchini










Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akisalimiana na Mwakilishi Mkaazi wa UN Umoja wa mataifa nchini Tanzania Dk. Alberic Kacou,alipofika Ikulu Mjini Zanzibar jana.





Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza na Mwakilishi Mkaazi wa UN Umoja wa mataifa nchini Tanzania Dk. Alberic Kacou,alipofika Ikulu Mjini Zanzibar jana.





Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza na Mwakilishi Mkaazi wa UN Umoja wa mataifa nchini Tanzania Dk. Alberic Kacou,alipofika Ikulu Mjini Zanzibar jana.(Picha na Ramadhan Othman Ikulu)

















Rais Zanzibar, Dk. Shein ateta na Watendaji wa Wizara za Kilimo na Maliasili, Mifugo na Uvivi















Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein,akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Kilimo na Maliasili,katika hatua zake za utekelezaji wa kazi za Wizara hiyo,ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar Januari 30.2012.













Watendaji wa Uongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein,alipozungumza nao katika ukumbi wa mikutano Ikulu Mjini Zanzibar, katika hatua zake za utekelezaji wa kazi za Wizara hiyo.(Picha na Ramadhan Othman Ikulu).
JK abariki posho mpya za wabunge





Rais Jakaya Mrisho Kikwete

KILA MMOJA KULIPWA 330,000 KWA SIKU, ZITTO, MAKAMBA, KIGWANGALA WASULUBISHWA KWA KUZIPINGA


Waandishi Wetu, Dodoma


WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesema tayari Rais Jakaya Kikwete amesaini kuidhinisha ongezeko la posho za vikao (sitting allowance) kwa wabunge kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000 kwa siku. Kupitishwa kwa posho hizo ambazo ziliandikwa kwa mara ya kwanza na gazeti hili, kunafanya sasa mbunge kupokea Sh330,000 kwa siku; Sh200,000 zikiwa ni posho ya kikao, Sh80,000 posho ya kujikimu na Sh50,000 nauli.


Taarifa za uhakika kutoka ndani ya kikao cha utanguzi cha wabunge jana, zilidai kuwa baada ya Pinda kutoa taarifa hiyo, wabunge walishangilia huku Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, akisimama na kudai kuwa taarifa alizonazo ni kwamba Rais Kikwete alikuwa hajasaini kuidhinisha posho hizo.


Hatua hiyo ilisababisha Mbunge wa Kondoa Kaskazini, Juma Nkamia (CCM), kusimama na kuhoji iwapo Zitto ni miongoni mwa wasemaji wa Rais kabla ya Pinda kusimama na kuthibitisha kusainiwa kwa posho hizo akisema siyo ajabu kwani hata watumishi wa Serikali wanalipwa kati ya Sh150,000 na Sh200,000. Hata hivyo, Zitto alitetea msimamo wake kwamba alitarajia baada ya kusainiwa kwa posho hizo na Rais, angepewa masharti mapya ya kazi za ubunge.



Katika kikao hicho baadhi ya wabunge wanadaiwa kuwashambulia Zitto, Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba na Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Khamis Kigwangwala kwamba wamekuwa mstari wa mbele kupinga posho hizo hadharani. Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye anadaiwa kwamba aliungana na Pinda kuthibitisha kwamba Rais Kikwete ameidhinisha posho hizo mpya, pia aliwashambulia wabunge wanaozipinga akisema kwamba wanafuta umaarufu wa kisiasa.


“Wanachotafuta ni umaarufu wa kisiasa tu, mimi ninavyojua umaarufu wa kisiasa unakuja kwa kufanya kazi za kibunge za wananchi lakini siyo kupinga posho,” chanzo chetu cha habari kilimnukuu Makinda.









Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa anadaiwa kwamba alitumia mafumbo kuwashambulia wabunge hao ambao wamejitokeza kupinga nyongeza hiyo ya posho. Kauli hiyo inadaiwa kuungwa mkono na Mbunge wa Sikonge (CCM), Said Nkumba ambaye alidai kuwa hawezi kumsemea Zitto kwa sababu ni kawaida yake kupinga, lakini akaelekeza shutuma zake kwa Makamba kwamba ameanza kupinga baada ya kugharamiwa na CCM. “Januari anapinga posho hizo kutokana na CCM kumpa gari, nyumba na analipwa na chama,” kilisema chanzo chetu kikimkariri Nkumba.










Pia, Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo (CCM), anadaiwa kumshambulia Zitto kuwa lazima apinge posho hizo kwa sababu, anapewa fedha na wafadhili kutoka nchi za nje. “Shelukindo anasema amefanya ziara nje na kuhakikisha kuna wahisani wanamfadhili Zitto kwa hiyo ana haki ya kupinga posho hizo,” chanzo chetu hicho kilimkariri Shelukindo.







Hata hivyo, inadaiwa kuwa baada ya mashambulizi hayo, Dk Kigwangwala alisimama kutetea msimamo wake kwamba ongezeko hilo halina ‘mashiko’ na haliwezi kuelezwa mbele ya umma likaeleweka, lakini alizomewa na wabunge wengi huku wakimtaka kukaa chini.










Hatua hiyo ilisababisha Zitto kusimama na kueleza kuwa tatizo la wabunge kwamba wana fikra finyu, kauli ambayo alitakiwa na wenzake kuwaomba radhi kuwa amewatukana. “Zitto ametumia Kiingereza kuwa tatizo la wabunge ‘we think small’, Shelukindo na (John) Komba wakaja juu wakitaka kuwaomba radhi kwa kuwatukana,” chanzo chetu kilieleza. Zitto anadaiwa kusema wabunge walitakiwa kujenga hoja ya kuongeza fedha za mafuta ya gari wanayolipwa hivi sasa Sh2.5 milioni kwa mwezi, kutokana na kupanda kwa nishati hiyo, lakini siyo posho.




Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alinukuliwa akisema matatizo ya posho yamefikia hapo baada ya kuonekana ni ya watu binafsi siyo mfumo hivyo, wanaopinga wanaonekana kama wanatafuta umaarufu na wana vipato vya fedha, akaitaka kamati ya uongozi ijadili na kupata mwafaka badala ya wajumbe kutofautiana mbele ya umma. Wabunge wengine wanaodaiwa kutetea posho hizo ni Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini na Jenister Mhagama (Peramiho CCM).


Msimamo wa January


Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Makamba alijibu: “Si sahihi kwangu kutoa taarifa za kikao cha ndani. Lakini msimamo wangu kwenye suala hilo unajulikana na haujabadilika. Msimamo wa CCM ulishawekwa wazi na sote tunaujua. Nitalizungumzia suala hili kwa kirefu katika siku zijazo.”

Kuhusu taarifa kwamba anagharamiwa na CCM, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo na badala yake kutaka kiulizwe chama hicho.



Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa kuhusu taratibu za kuwagharamia viongozi wa chama chake ambao ni wabunge alisema: “Mbunge au kiongozi yeyote wa chama mwenye nafasi nyingine anagharamiwa na chama pale anapokwenda kufanya shughuli za chama tu na si vinginevyo.”


“Kwa hiyo kama ni mbunge suala la mafuta, dereva, mahali pa kulala na mahitaji mengine anagharamiwa na taasisi anayoifanyia kazi na siyo chama.”


“Kwa mfano, mimi kwenye sekretarieti hata posho za vikao huwa sichukui, nadhani na mwenzangu January naye sidhani kama huwa anachukua posho, kwa sababu tukifanya hivyo ni kama tunakiumiza chama, huo ndiyo msimamo wetu na uko wazi wala siyo kificho.”


Kwa upande wake, Zitto alisema jana kwamba hakuwa katika nafasi ya kuzungumzia suala hilo na badala yake kuahidi kwamba atalizungumza leo atakapokutana na waandishi wa habari.


Wabunge walia njaa

Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zilisema wabunge hao walilalamikia kucheleweshwa kulipwa posho zao za wiki mbili walizokaa Dar es Salaam wakati wa vikao vya kamati.

Walidai hivi sasa wanaishi kwa shida huku wakihoji sababu za kucheleweshewa.

Imeelezwa kwamba Spika Makinda alidai kuwa fedha hizo zipo na kwamba kilichochelewesha ni uhakiki wa wabunge waliohudhuria vikao.


Makinda alisema baadhi ya wabunge wamekuwa wakilipwa posho za vikao bila kuhudhuria, hatua ambayo imesababisha Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG), kuhoji maswali mengi.

CHANZO: Mwananchi




201 WAAGA DUNIA KUTOKANA NA MGOMO WA MADAKTARI





Makongoro Oging’ na Haruni Sanchawa
MGOMO wa madaktari unaoendelea nchini tangu Jumatatu ya wiki iliyopita, inasemekana umesababisha vifo vya wagonjwa wanaokadiriwa kufikia 201.



Uchunguzi uliofanywa na timu ya Uwazi tangu mgomo huo ulipoanza, umegundua kwamba kiasi hicho cha wagonjwa waliokufa ni katika mikoa inayokabiliwa na tatizo hilo la madaktari kugoma.
Waandishi wetu Dar es Salaam, walitembelea wodi kadhaa na vyumba vya kuhifadhia maiti vya Hospitali za Temeke, Amana, Mwananyamala na Muhimbili kujionea athari za mgomo huo, huku wa mikoani nao walifanya hivyo.



MUHIMBILI
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, umebaini kuwa wagonjwa wengi wameathiriwa na mgomo huo hali iliyowafanya wajazane wodini bila kupata tiba.
Aidha, timu yetu ilishuhudia wagonjwa wengi wakiwa wamelala chini kwenye korido huku wakiugulia maumivu kwa kukosa huduma ya madaktari.



Akizungumza na gazeti hili wiki iliyopita mmoja wa wagonjwa aliyejitambulisha kwa jina la Samson Maandizi, aliyelazwa Wodi ya Sewahaji alisema tangu alipofika hospitalini hapo kutokana na majeraha aliyoyapata katika ajali ya gari, hajawahi kupata matibabu.
Kufuatia hali tete ya kimatibabu iliyosababishwa na mgomo huo, baadhi ya wananchi wamelazimika kuwahamisha wagonjwa wao na kuwapeleka katika hospitali binafsi.



Hata hivyo, mwananchi mwingine, Hamisi Juma alipohojiwa na gazeti hili hospitalini hapo alisema: “Kutokana na kutokuwa na fedha nimeamua kumhamisha mama yangu na kumpeleka kwa mganga wa kienyeji Mbagala.” Kwa upande wa chumba cha kuhifadhia maiti hospitalini hapo, mhudumu ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema kwamba tangu mgomo huo uanze idadi ya waliokufa mpaka juzi (Jumapili) wanaweza kufikia 57.

MWANANYAMALA
Kwa upande wa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mwananyamala, mmoja wa wahudumu alisema kwamba idadi ya waliokufa kwa kipindi hicho wanaweza kufikia 20.

AMANA
Katika Hospitali ya Amana mhudumu wa chumba cha maiti amesema tangu mgomo huo ulipoanza, watu waliofariki wanaweza kufikia 15.

TEMEKE
Nayo Hospitali ya Temeke hali ni tete kwani inadaiwa nako wagonjwa 19 wamefariki dunia kipindi cha mgomo, kwa mujibu wa mtumishi mmoja wa hospitali hiyo.

BUGANDO MWANZA
Katika Hospitali ya Bugando Mwanza, mmoja wa wahudumu wa chumba cha maiti alimwambia mwandishi wetu mjini humo kwamba kipindi hiki cha mgomo, wagonjwa waliofariki wanaweza kufikia 25.

MBEYA
Mwandishi wetu wa Mbeya, Gordon Kalulunga, anaripoti kuwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoani humo wagonjwa wanaofikia 22 walipoteza maisha na wengine walitoroshwa na ndugu zao wakiwa na dripu baada ya kuona hali zao ni mbaya.

DODOMA
Mwandishi wetu Dodoma anaripoti kuwa mgomo huo umesababidha adha kubwa kwa wagonjwa na inakadiriwa watu tisa wamefariki dunia huku wengi wakirudishwa majumbani kwao.

MOROGORO
Mwandishi wetu, Dunstan Shekidele anaripoti:
Kwa mujibu wa mhudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Morogoro aliyeomba jina lake lihifadhiwe, watu wanaokadiriwa 14 wamefariki dunia tangu mgomo huo ulipoanza.
“Kuna baadhi ya ndugu wamewaondoa wangonjwa wao wakiwa na dripu, kwa kweli hali ni mbaya, tumeambiwa wengine wanafia majumbani,” alisema mhudumu huyo.

KIGOMA, IRINGA NA TANGA
Waandishi wetu katika mikoa hiyo wameripoti vifo idadi yake katika mabano kama ifuatavyo;
Kigoma (nane), Bombo mkoani Tanga (nane) na Iringa (saba).
Hata hivyo, Waziri Mkuu, Mizengo Kayanza Pinda ilikuwa akutane na madaktari Jumapili iliyopita kuzungumzia mgogoro huo lakini ikashindikana kwani Mwenyekiti wa Madaktari, Ulimboka Stephen aliliambia gazeti hili kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ilichelewesha barua ya mwaliko.
Madaktari hao wameitisha mgomo wakidai kuongezewa posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu hatarishi , nyumba na usafiri wa kwenda na kurudi kazini.SOURCE: GLOBAL PUBLISHERS TZ


































No comments:

Post a Comment