Wednesday, September 26, 2012

WATALII WAFURIKA SERENGETI KUSHUHUDIA MSAFARA WA NYUMBU UKIREJEA NYUMBANI HIFADHI YA TAIFA YA SERENGETI WAKITOKEA MAPUMZIKO YA MWEZI MMOJA KENYA


Kila mwaka, nyumbu pamoja na wanyama wengine kama pundamilia na swala hufanya mzunguko maalum unaochukua miezi 12 ya mwaka ambapo miezi kumi kati ya hiyo huwepo nchini katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na iliyobaki hutumiwa na wanyama hao katika eneo la Hifadhi ya Masai Mara nchini Kenya.


Mwaka huu msafara huu unaohusisha wanyama zaidi ya Milioni Moja na Nusu na ambao hutembea katika mzunguko wa takribani Kilometa 1,000 umewahi sana kurejea nchini ukitokea mapumziko.

Kwa mujibu wa taarifa za kitaalamu hali hii inatokana na kuwahi kunyesha kwa mvua katika eneo la Serengeti ambapo imesababisha kuwepo na nyasi nzuri ambazo ni chakula muhimu kwa wanayama hawa.


Changamoto kubwa wanayokutana nayo msafara huu mara unaporejea nyumbani ni tukio la kuvuka Mto Mara ambao umejaa wanyama wakali aina ya mamba na viboko ambao nao huwa ni msimu wao wa kujipatia chakula kwa kuvizia na hatimaye kuwakamata wanyama hawa mara wanapovuka mto.


Watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani wamekuwa wakifurika katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kushuhudia tukio hili adimu la kuvuka Mto Mara ambalo wengi wao wamekuwa wakiliona kupitia filamu mbalimbali zilizotengenezwa katika eneo hili.


Source;Michuzi Blog

No comments:

Post a Comment