Pages

Monday, March 4, 2013

Tanzania yatukanwa na Muingereza, huku wakubwa wakizubaa


Sarah Hermitage
 Ms Sarah Hermitage

KWA takriban miaka mitano sasa, raia mmoja wa Uingereza, Sarah Hermitage amekuwa akiendesha kampeni ya kumchafua Rais Jakaya Kikwete, Serikali ya Tanzania, taasisi muhimu za nchi yetu kama vile mahakama, waandishi wa habari na hata Watanzania ambao wamekua wakimpinga.
Pamoja na kuwa kumekua na mapungufu katika serikali yake na vyombo vyake kama ilivyo kwa serikali nyingine Duniani ikiwamo ya Uingereza, Muingereza huyu amekua akitoa kashfa kwa kila jambo linaloandikwa ama kujadiliwa kuhusiana na viongozi wa Tanzania na taasisi zake na kwa kutumia lugha isiyo na staha.
Watanzania siku zote wakiwamo wanasiasa, waandishi wa habari na wanaharakati, wamekua wakiikosoa na hata kuishambulia serikali na vyombo vyake inapokosea jambo ambalo ni jema na linasaidia kuimarisha utawala bora, lakini kwa staili anayotumia Muingereza huyu ni kupitiliza mipaka na zaidi ya yote ni udhalilishaji usioweza kuvumilika kwa mtu mwenye mapenzi mema na nchi yake.
Dhumuni la Sarah Hermitage na washirika wake wakiwemo baadhi ya Watanzania ni kuzishawishi nchi za Magharibi wakianzia na Uingereza kusitisha misaada na uwekezaji katika Tanzania. Hilo angeweza kulifanya huko kwao kwa kuwasiliana na serikali yake, lakini badala yake amekuwa akitumia mitandao ya kijamii na barua pepe tena kwa kutumia lugha ya kukashifu na kudhalilisha. 
Watanzania wote tuna jukumu la kutetea heshima ya nchi yetu, lakini wapo wale ambao tumewapa jukumu la kusimama mstari wa mbele. Jambo la kusikitisha ni kwamba ni watu wachache sana kama Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe ambaye ambaye amekua na ujasiri wa kumkabili Muingereza huyu, kwa kumwambia wazi kwamba kama ni misaada ana haki ya kuishawishi nchi yake kuzuia misaada kwa Tanzania lakini si kwa kudhalilisha Watanzania.
Zitto alienda mbali zaidi kwa kusema kwamba nchi nyingi tajiri duniani ikiwamo Uingereza, zimejengwa kwa kutumia rasilimali walizozipora katika nchi walizozitawala ikiwamo Tanzania na kwamba nchi hizo zinaweza pia kuendesha shughuli zake bila misaada ya dharau. Bahati mbaya sana watendaji wengine wengi ambao wanapaswa kutetea heshima yetu, hili suala limewapita, pengine kutokana na kutokua na taarifa sahihi ama kwa kutowajibika.
Jambo la kujiuliza, wale ambao miongoni mwa majukumu yao ya kila siku ni kutetea na kulinda hadhi na heshima ya nchi yetu wanafanya kazi gani? Sasa tunawalipa mishahara mikubwa na marupurupu ya nini kama hawawezi kututetea tunapodhalilishwa ama kutukanwa? 
Hali hii inatufanya tukumbuke ujasiri wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye mara kadhaa aliwatunishia misuli viongozi wa mataifa makubwa walipotaka kuidhalilisha nchi yetu, sembuse raia mmoja ambaye amekua akitumia matatizo yake binafsi kutaka kuidhalilisha Tanzania na kutaka kuishinikiza serikali yake na nyingine kuichukia Tanzania.
Jinsi anavyotumia mtandao wa twitter kuchafua Tanzania
Sarah Hermitage amekua akitafuta katika taarifa za vyombo vya habari vya ndani na nje ya Tanzania vinavyoandika taarifa zozote kuhusu Tanzania na kuziongezea maneno ya kukashifu na kejeli. 
Kwa mfano amekua amechukua taarifa inayomunukuu Raia Jakaya Kikwete akiitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kupambana na rushwa hadi ndani ya Baraza la Mawaaziri, na yeye kuongezea maneno akisema, “kundi moja la majambazi linaliambia kundi lingine la majambazi kukamata mwizi”.
Akachukua taarifa iliyochapishwa katika vyombo vya habari ikimnukuu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akikaribisha wawekezaji katika kilimo na yeye kuongeza maneno akisema, “Mheshimiwa Pinda kitakachoendelea kukandamizi uwekezaji katika kilimo cha Tanzania ni uporaji wa ardhi ya wawekezaji katika mtindo wa Mugabe (Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe).”
Amekua akidiriki kukashifu hadi majaji wote wa Tanzania kwamba wana bei akisema, “sina hakika kama unaweza kupata jaji ambaye si mla rushwa. Wote wana bei,” kauli ambayo hata Watanzania wanakua wakiitoa kwa uangalifu maana hata kama kuna majaji ambao si waadilifu, haiwezekani wakawa ni wote, kama ilivyo katika taasisi nyingine.
Raia mmoja wa Kenya anayeishi Tanzania, aliyejitambulisha kwa jina la Marigi Patrick aliandika katika mtandao kwa kusema; 
“Sisi Wakenya tuna matatizo yetu na tumekua na tofauti kubwa sana za wazi wazi, lakini anapotokea raia wa kigeni kumshambulia kiongozi wetu tena kama Rais wa nchi, tunaungana na kumshughulikia. Kuna wakati Wazungu walimshambulia Rais Mwai Kibaki, sote tukisaidiwa na wabunge wetu na vyombo vya habari tulimshambulia hadi akakoma kutudharau.”
Marigi ambaye anajihusisha na biashara ya bima, anasema Watanzania bado ni wachanga katika demokrasia, ama wanadharau kila kitu bila kujua madhara yake katika hadhi na heshima ya Taifa, na ndio maana wanashindwa kutofautisha kati ya demokrasia na udhalilishaji unaofanywa na raia wa nchi nyingine kama alivyo Sarah Hermitage. 

Source:  THE SILVER DALE CASE BLOG

No comments:

Post a Comment